THE DREAM STUDIOS

wambura babu log

DARDYS FASHION

DARDYS FASHION

Tuesday, 23 December 2014

Neno La Leo: Rais, Utu Na Haki...

Kwenye Jamhuri Rais ana mamlaka makubwa sana, Hivyo, kwenye Jamhuri, Rais aweza kuwa dikteta, akitaka. Anaweza kuonea na hata kukandamiza raia wake. Kuwanyima haki.
Kwenye nchi yetu hatujapata bahati mbaya ya kuwa na Rais dikteta. Na hata wale wenye kutamani Rais dikteta, kimsingi hawajawahi kuishi kwenye utawala wa rais dikteta.
Na yanayoitwa maamuzi magumu ya Rais kwenye Jamhuri yaweza pia kutafsiriwa kama maamuzi ya kidikteta. Kinachotakiwa ni maamuzi yenye hekima na busara. Na mwenye kutanguliza hayo, maamuzi yake husemwa pia kuwa ni magumu. Maana, si kazi rahisi kufikia maamuzi yenye hekima na busara. Maamuzi yenye kuzingatia Utu na Haki.

Rais kwenye Jamhuri anapaswa kuwa kielelezo cha Utu na Haki. Maana, Rais kwenye Jamhuri yumkini ni kimbilio la mwisho la mnyonge, na mwenye nguvu pia. Ni kwenye kudai haki yake anapoona ameikosa kwengineko.
Kwenye utawala wake, Mzee Ali Hassan Mwinyi alianzisha utaratibu wa kukutana na wananchi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kwenye ofisi ndogo za CCM, Lumumba. Mzee Mwinyi alitambua, kuwa miongoni mwa aliowaongoza, kuna wanyonge na hata wenye nguvu, waliokoseshwa haki zao kwenye mifumo ya kawaida, na hawakuwa na pakukimbilia, isipokuwa kwa Rais wa Nchi.
Ndio, kwenye Ikulu za Afrika, zenye kukaliwa na Marais wenye kuthamini Utu na Haki za raia wao, kila kukicha, utawakuta raia, wengine wamesafiri kutoka umbali mrefu, wametaka waelekezwe iliko Ikulu, ili wao wenyewe, wamfikishie Rais kero zao.
Ndio maana ya kusema, Katika Nchi, Rais ni kielelezo cha Utu na Haki.
Ni Neno La Leo.
Maggid,
Mji Mkongwe, Zanzibar.