


Wastaafu wa
Taasisi za Umma za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na zile
za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wanapaswa kushirikiana kwa karibu
katika kutumia ujuzi na Taaluma zao za muda mrefu ndani ya Jumuiya
wanazozianzisha baada ya kustaafu kwao ili waendelee kuchangia
Maendeleo ya Taifa.
Kauli hiyo
imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
wakati akiizindua rasmi Bodi ya wadhamini ya Jumuiya ya Wastaafu Pemba
hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Tasaf uliopo katika Majengo ya
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar yaliyopo Chake chake Pemba.
Balozi Seif
alisema mashirikiano hayo yatatoa nafasi nzuri kwa wastaafu hao kuondoa
shaka ya kuendeleza maisha yao kwani baadhi yao hupata wakati mgumu
kabla na baada ya kustaafu kwa vile wanakuwa bado hawajajipanga.